Header Ads Widget

JACQUELINE MENGI AFUNGUKA BAADA YA UAMUZI WA MAHAKAMA JUU YA MIRATHI YA MUMEWE



Jacqueline Ntuyabaliwe, mjane wa Reginald Mengi amesema mumewe hakuwa na matatizo ya akili kama inavyodaiwa na kuwataka wanaotoa madai hayo kuacha uzushi.

Ameeleza hayo kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, ikiwa zimepita siku tatu tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuukataa wosia uliokuwa ukidaiwa kuandikwa na Mengi ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu nchini ambapo pamoja na mambo mengine ikieleza kuwa haukidhi matakwa ya kisheria ili kuwa wosia halali.

Katika maelezo yake aliyoyatoa jana Alhamisi Mei 20, 2021 mlimbwende huyo wa Tanzania mwaka 2000 amesema wanaoibua uzushi huo wanaweza kusema chochote wanachojisikia na kuchukua mali zote lakini hawezi akakaa kimya na kuacha wamchafue Mengi, atasimama na kumtetea katika hilo.

“Hii ni ripoti yake ya hospitali, huu ni kweli kwa wale ambao wanataka kupata uhakika. Mume wangu hakuwa na matatizo ya kiakili.”

“Mnaweza mkasema chochote mnachojisikia na kuchukua kila kitu lakini kwa hili nitamtetea hadi umauti wangu utakaponifika. Daktari Kaushik Ranchod kutoka Afrika Kusini na daktari Anthony Rudd kutoka Uingereza wanaujua ukweli kuhusu hili,” amesema Jacqueline aliyeambatanisha picha ya ripoti ya hospitali ya Mengi aliyefariki dunia Mei 2, 2019.

Uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa Jumanne Mei 18, 2021 na Jaji Yose Mlyambina kufuatia shauri la mirathi lililokuwa limefunguliwa na watu wanne wakiwemo ndugu wa marehemu, wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi hiyo.

Jaji Mlyambina amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na mmoja wa watoto wakubwa wa marehemu Mengi pamoja na ndugu yake marehemu Mengi, waliokuwa wakipinga uhalali wa wosia huo.

Shauri hilo la mirathi namba 39 la mwaka 2019 lilifunguliwa na Benson Benjamin Mengi, William Onesmo Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Novatus Mushi wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi mirathi hiyo kwa mujibu wa wosia huo.

Hata hivyo, mtoto wa marehemu Mengi, Abdiel Reginald Mengi na ndugu wa Mengi, Benjamin Abraham Mengi, waliweka pingamizi dhidi ya wosia huo, wakipinga uhalali wake huku wakiwasilisha jumla ya sababu nne za kuupinga.

Sababu hizo ni pamoja na kwamba haukwa umepigwa mhuri na saini iliyokuwepo ilikuwa ni tofauti na saini ya kawaida ya marehemu Mengi na kwamba haukushuhudiwa na ndugu au mke wa marehemu.

Pia walikuwa wakidai kuwa marehemu hakuwa na uwezo wa kuandaa wosia kwa kuwa alikuwa na matatizo ya kiafya tangu mwaka 2016 na kwamba unaondoa katika urithi, watoto bila kuzingatia mila za Kichaga au kuhusisha ndugu.

SOMA ZAIDI HAPA


Post a Comment

0 Comments