Header Ads Widget

BAADHI YA WANAWAKE KATA YA MWAMALA SHINYANGA WAELEZA WANAVYONYIMWA FURSA YA KUSHIRIKI VIKAO, UONGOZI

Wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakifuatilia semina iliyokuwa ikitolewa katika kata hiyo

Na Suzy Luhende -Shinyanga 
WANANCHI wa Kata ya Mwamala halmashari ya wilaya ya Shinyanga vijijini wamesema hali ya ukatili wa kijinsia imepungua vijijini, lakini bado tatizo lipo kwa baadhi ya wanaume ambao wanaendekeza mila na desturi ya kuwanyima wanawake haki ya kuchangia jambo katika vikao vya kifamilia kwenye vikao na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao, wamesema hali ya ukatili bado ni changamoto kwani wanaume bado wanaendekeza mira na desturi za kuwaona wanawake kuwa hawawezi kutoa maamzi yeyote katika familia na katika vikao mbalimbali vya kijamii.

Baadhi ya wananchi hao  akiwemo Salome Dotto mkazi wa Kijiji cha Bunonga Kata ya Mwamala na Magesa Mwandu mkazi wa kijiji cha Mwamala wamesema kuwa akina mama bado wanafanyiwa ukatili na waume zao kwa kukatazwa kuzungumza kwani hata kuchangia neno kwenye maongezi ya familia hatakiwi.

"Hata kwenda kwenye vikao vya kijamii ni tatizo wanaambiwa wakae nyumbani wapikie watoto wanaume ndio wanaotakiwa kwenda kwenye vikao mbalimbali vinavyojitokeza katika kijiji, hata baadhi wanaoenda kwenye vikao hawatakiwi kuchangia neno lolote akithubutu tu huyo akirudi nyumbani anapigwa na mme wake kuwa ana kihelehele, ndio maana wanawake hawazungumzi ukimuona kazungumza labda alishaolewa na kuachika ndiyo anaweza kutoa hoja," amesema Dotto.

"Wanaume wanasema eti sisi wanawake tukigombea nafasi za uongozi tutakuwa malaya, ndiyo maana wanatukataza wanasema kazi yetu sisi ni kukaa na kulea watoto, wenyewe ndio wataenda kwenye vikao vyoyote vitakavyojitokeza, na mkija kuwauliza kwamba mmeambiwahuko wanawajibu kuwa hayatuhusu, hivyo tunanyamaza bila kujua kinachoendelea katika kijiji au katika kata," amesema Maria Petro.

Naye Kashinje Zunzu mkazi wa kata ya Mwamala amesema kweli ukatili wa kutompa nafasi mwanamke azungumze katika familia haupo kwa wanaume wengi, lakini kutokana na elimu inayotolewa kwa sasa baadhi ya wanaume wanabadilika, hivyo ni vizuri elimu iendelee kutolewa mara kwa mara ili jamii iweze kubadilika.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Agnes Ginethon amesema wanaume kweli wamekuwa wakiwashirikisha tu wanawake kwenye kulima na kuvuna lakini kwenye kuuza wanaume hawawapi nafasi ya kuzungumza, hivyo wanajichukulia maamzi wao wenyewe kuuza mazao ambayo walilima wote mme na mke.

"Mwanamke hata kwenda kugombea nafasi za uongozi haruhusiwi kwa kuendekeza mila na desturi, wanaume mnatakiwa kubadilika kwani mwanamke akipata nafasi yeyote ya uongozi mnasaidizana na mnatakiwa kuwapa nafasi kina mama ya kuchangia mawazo yao katika kufanya maendeleo ya kifamilia na maendeleo ya kijamii kwani mnapowakataza mnawafanyia ukatili wa kisaikolojia"amesema Agnes.

Agnes amesema ili kutokomeza ukatili Women Fund Tanzania (WFT) imetoa kiasi cha fedha kwa halmashari ya Shinyanga na kwa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kupitia mradi wa nafasi ya vyombo vya habari kwa ajili ya kuelimisha jamii ya Shinyanga na kutokomeza ukatili wakijinsia wilayani humo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwamala, Suzan Kayange amesema hali hii ya ukatili bado inaendelea kwenye jamii kwani hata wananchi wote wakialikwa kwenye kikao wanaume wanajitokeza wengi lakini wanawake ni wachache na wanaozungumza sana ni wanaume wanawake wananyamaza kimya kama vile hawapo.
 Wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Kaselya kata ya Mwamala akichangia jambo juu ya ukatili wa kijinsia katika kikao cha wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili


TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807