Header Ads Widget

FAMILIA YA MAREHEMU YAREJESHEWA NYUMBA ILIYOPORWA NA MFANYABISHARA WA MIKOPO UMIZA, DC MACHA AAHIDI MSAKO KWA WENGINE

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (kulia) akimkabidhi nyaraka za umiliki wa nyumba mtoto wa marehemu Rose Edward ambayo ilikuwa imeuzwa kinyemela.

Na Salvatory Ntandu, Kahama
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kahama imeirejeshea familia ya marehemu Edward Mpolosi nyumba iliyopo katika kitalu J 165 mtaa wa Nyihogo iliyokuwa imechukuliwa kinyume cha utaratibu na mfanyabiashara wa mikopo umiza aliyetambulika kwa jina la  Masero Nyamhanga.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Kahama, Frank Masilamba, utaratibu uliotumika kujimilikisha nyumba hiyo Mfanyabiashara huyo ulikuwa batili na haukuzingatia sheria.

“Marehemu Edward alichukua mkopo wa Sh 300,000 lakini alipochelewesha kulipa deni hilo liliongezeka riba hadi kufikia Sh Milioni 10,500,000 ndipo alilazimika kuingia mkataba batili wa mauziano ya nyumba hiyo huku mkopeshaji akijua wazi kuwa alikuwa anatenda kosa,”alisema Masilamba.

Alifafanua kuwa watoto wa Marehemu walifika katika ofisi za Takukuru kuhusiana na baba yao kudhulumiwa nyumba  walianza uchunguzi na kubaini kuwa makubaliano ya mauziano ya nyumba hiyo yalikuwa ni batili.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha alisema kuwa serikali imeamua kuikabidhi nyumba hiyo watoto wa Marehemu Edward ambao ni Rose na George ili waendelee kuimiliki baada ya Masero kubainika hana uhalali wa mauziano ya nyumba hiyo maelekezo.

“Hatutawavumilia wafanyabiashara wanaotumia fedha zao kunyanyasa wananchi wanyonge kwa kuwakopesha mikopo umiza ambayo imekuwa ikiendelea kupoka haki za watu wengine, tutaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaobainika kutoa mikopo umiza bila kufuata sheria za nchi,”alisema Macha.

Nae Rose Edward ambaye alikabidhiwa nyumba hiyo aliishukuru taasisi hiyo kwa kufanikiwa kuwarejeshea nyumba yao ambayo ilikuwa imetwaliwa kinyemela na familia ya Masero,mgogoro ambao umewasumbua kwa muda mrefu bila ya kupata mafanikio kutokana na mkopeji huyo kudai kuwa aliuziwa nyumba hiyo na marehemu baba yao.

“Tunaipongeza serikali kwa kutusikiliza sisi wanyonye baada ya baba yetu kufariki tulianza kupokonywa mali zake ikiwemo nyumba,tumeishi maisha ya shida kutokana na mgogoro wa nyumba yetu ambayo leo tumeirejeshewa,”alisema Rose.


Post a Comment

0 Comments