Header Ads Widget

15 WATIWA MBARONI WAKIUZIANA DHAHABU GESTI


JESHI la Polisi Mkoa wa Simiyu limekamata watu 15 wanaotuhumiwa kuuziana dhahabu kwenye nyumba ya kulala wageni katika mgodi wa dhahabu Lubaga namba mbili uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Richard Abwao alisema jana kuwa, watu hao walikamatwa Januari 13, mwaka huu, saa 1:00 usiku wakiwa na dhahabu yenye uzito wa gramu 9.2.

Kamanda Abwao aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa kwenye nyumba hiyo wakifanya biashara ya kuuziana madini hayo kinyume cha sheria.

“Askari wetu wakiwa doria kwenye mgodi huo waliwakuta watu hawa wakifanya biashara hiyo kwenye nyumba ya kulala wageni ambayo ipo ndani ya mgodi huo, sheria inataka biashara ifanyike kwenye soko la madini.”

“Na kwenye mgodi huo kuna soko la madini ambalo limeanzishwa na serikali linalotumika kuuzia madini, lakini hawa walikuwa sehemu ambayo siyo sahihi na lengo lao lilikuwa kukwepa kulipa kodi ya serikali,” alisemqa Kamanda Abwao.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kukamata watu hao na kueleza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho.

“Serikali imeweka soko kwenye ngodi huo litumike kwa ajili ya kuuzia madini, lakini bado kuna watu wanaendelea kuuziana vichochoroni.”

“Vyombo vyote vipo kazini, tutaendelea kuwakamata maana tunazo taarifa wapo wengine tutawakamata wote, niwaombe watu kwenye mgodi huu waache mara moja tabia hii kwani hatutakuwa na mzaha kwenye hili,” alisema Kiswaga.

Post a Comment

0 Comments