Header Ads Widget

TUME YA USHINDANI YAWAFUNZA WENYE ULEMAVU WA KUSIKIA KAHAMA NAMNA YA KUTAMBUA BIDHAA BANDIA

Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya (aliyeinua mkono) akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya majukumu ya Tume ya Ushindani (FCC) na namna ya kutambua bidhaa bandia kwa watu wenye ulemavu wa kusikia wilayani Kahama, iliyofanya leo katika Ukumbi wa Niteshi mjini Kahama. (Picha: Mpiga picha wetu)

Na Damian Masyenene –Kahama
KUNDI la watu wenye ulemavu wa kusikia nchini ambalo linakadiriwa kuwa na watu zaidi ya 596,000, limekuwa likikumbana na changamoto ya kutambua bidhaa bandia sokoni na kujikuta likiwa mhanga wa udanganyifu wa wafanyabiashara waongo wanaotumia mwanya huo kuwatapeli.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo na kuhakikisha watu wenye ulemavu wa kusikia wanafanya ujasiriamali katika mazingira rafiki, Tume ya Ushindani (FCC) imetoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga juu ya majukumu ya tume hiyo na udhibiti bidhaa bandia ili waweze kubaini na kutofautisha bidhaa zisizofaa. 

Mafunzo hayo yametolewa leo Novemba 26, 2020 katika Ukumbi wa Niteshi mjini Kahama yakishirikisha watu wenye ulemavu wa kusikia 65 ili kuwalinda dhidi ya mienendo hadaifu, gandamizi na potofu katika soko la biashara ya bidhaa mbalimbali. 

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya ametoa wito kwa vyama vingine vya watu wenye ulemavu vinavyojishughulisha na masuala ya ujasiriamali kutafuta elimu hiyo kutoka Tume ya Ushindani (FCC) na idara nyingine za Serikali kwa ajili ya ustawi wa biashara na usimamizi wa soko nchini na kuwezesha kupiga hatua katika kuanzisha, kulea na kukuza biashara zao. 

Pia amebainisha kuwa wilaya ya Kahama imeanzisha kitengo cha kuwawezesha wananchi kiuchumi katika eneo la Nyihogo wilayani Kahama, ambapo amewahimiza wajasiriamali katika kundi hilo kuitumia fursa hiyo kujiinua kiuchumi, huku akiwataka wajasiriamali wote kuzingatia maadili ya biashara ili kuhakikisha soko linabaki kuwa la ushindani, bidhaa zinazopelekwa sokoni zinakidhi matarajio ya walaji au wateja na taratibu za kupata faida zinazingatia na kuthamini utu wa mtu. 

“Napenda kuwatia shime Tume ya Ushindani kuendelea kupeleka elimu hii ya udhibiti wa bidhaa bandia kwa makundi mbalimbali yenye uhitaji maalum hususan kundi hili la walemavu wa kusikia, na ni matarajio yangu kuwa wanasemina mtaipeleka elimu hii kwa wenzenu na kuwasilisha kero na changamoto mnazokabiliana nazo katika shughuli zenu ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na ushauri stahiki,” amesema Ndanya. 

Akitoa neno kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Mkurugenzi Udhibiti Bidhaa Bandia, Godfrey Gabriel amesema kundi hilo la watu wenye ulemavu ni kundi muhimu katika kulilinda na bidhaa bandia sokoni ikizingatiwa kuwa mkoa wa Shinyanga ni njiia ya mwingiliano na mataifa jirani, ambapo ameomba ushirikiano kwa makundi mbalimbali na taasisi kudhibiti bidhaa mbandia na kuziondoa sokoni. 

“Utetezi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia ni juhudi muhimu katika kuimarisha mtangamano mzuri wa biashara katika soko na kuvutia wawekezaji haswa wa viwanda, kupitia elimu hii naamini italeta mchango chanya katika kudhibiti bidhaa bandia sokoni na kuondoa udanganyifu kwa walemavu wanapofanya biashara,” alisema. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) Mkoa wa Shinyanga, Zawadi Mashudi amesema kuwa viziwi wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa wakati wa kufanya manunuzi na kutambua bidhaa zisizofaa, ambapo wafanyabiashara wamekuwa wakitumia udhaifu huo kuwaonea na kuwauzia bidhaa zisizokidhi vigezo. 

Mashudi ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Wilaya ya Kahama na mjasiriamali wa vifaa vya Elektroniki, amesisitiza kuwa wamekuwa wakigombana na wateja kutokana na kuuziwa bidhaa bandia na wafanyabiashara wakubwa, ambapo ameiomba Serikali kuisambaza elimu kwa kundi hilo na kutambua changamoto wanazozipitia watu wenye ulemavu mbalimbali katika kuzitambua bidhaa bora. 

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Rehema Joshua ambaye ni Mwenyekiti wa idara ya Wanawake na Watoto, amesema kuwa sehemu kubwa ya wajasiriamali wenye ulemavu hawana elimu ya utambuzi wa bidhaa hususan wenye ulemavu wa kusikia wamekuwa wakionewa mara nyingi, huku akiishukuru Tume ya Ushindani kwa kuliona hilo na kutoa elimu na kuwasihi wale wanaokumbwa na uhuni huo watoe taarifa kwa mamlaka zinazohusika.
Mkurugenzi wa Udhibiti bidhaa bandia kutoka FCC, Godfrey Gabriel (kulia) akizungumzia umuhimu wa semina hiyo kwa kundi maalum la walemavu katika mkoa wa Shinyanga
Washiriki kutoka kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia wakipata elimu kutoka FCC
Mafunzo yakiendelea

Picha na Mpiga picha wetu

Post a Comment

0 Comments