Header Ads Widget

IGP SIRRO AWATAKA LISSU NA LEMA WARUDI, YUKO TAYARI KUWAPA ULINZI

IGP Simon Sirro

INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, amewataka wanasiasa waliokimbia nje ya nchi kwa madai ya kutishiwa usalama wa maisha yao kurejea Tanzania kwa kuwa kuna amani na yuko tayari kuwapa ulinzi.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Novemba 19, 2020 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam na kutoa tathmini ya jeshi hilo kuhusu hali ya usalama wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.

“Uchaguzi ulikwenda vizuri na nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wadau wote wa uchaguzi, viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa sana. Kuna watu walijipanga kufanya vurugu mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 kukamilika kwa maeneo yote ya Tanzania bara na visiwani, lakini jeshi la polisi tulibaini mapema na kudhibiti njama hizo.

“Jeshi la Polisi lilikamata watu na mabomu kadhaa visiwani Zanzibar, ambao walilenga kulipua ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), vituo vya mafuta pamoja na majengo makubwa ya serikali. Hali ya nchi yetu ni shwari sana hatuna matukio makubwa ya uvunjifu wa amani, kuna changamoto kidogo kwenye matukio haya ya udhalilishaji ambayo yanaoneka kuongezeka hasa makosa ya kubaka na kulawiti na makosa ya uhalifu yanazidi kupungua.

“Hakukuwa na maandamano ya amani yaliyopangwa, bali mtego wa kuliingiza taifa katika fujo, kuna baadhi ya viongozi wa Chadema, Tundu Lissu na wengine kama Godbless Lema walidai kutishiwa kuuawa jambo ambalo siyo kweli. Tanzania tuko salama, niwaambie tena Lissu na Lema na wengine waliokimbia nchi warudi, Tanzania iko salama waje tujenge nchi.

“Wakati ndugu yetu Tundu Lissu alipokwenda ubalozini akisema anatishiwa, niliandika barua aje basi atuambie anatishiwa na nani, lakini habari ya kutishiwa wewe unaweza ukagombana na mtu akakutishia, kama umetishiwa unatoa taarifa polisi. Jeshi la polisi lilimuita mara kwa mara Tundu Lissu aje atoe ushirikiano juu ya tukio lake la kupigwa risasi kule Dodoma, lakini hakutaka kufanya hivyo anapolisema Jeshi la Polisi linamuonea hii siyo sawa,” amesema Sirro.

Post a Comment

0 Comments