Header Ads Widget

RC TELACK, RPC MAGILIGIMBA WAONGOZA UZINDUZI WA MPANGO MKAKATI KUTOKOMEZA UKATILI KWA WANAWAKE SHINYANGA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akimkabidhi kitabu chenye mpango mkakati wa miaka mitano wa kutokomeza ukatili wa kijinsia, Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba kilichoandaliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Na Suzy Luhende - Shinyanga
SERIKALI mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imezindua mpango mkakati wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambao utadumu kwa muda wa miaka mitano, ili kuondokana na ukatili zikiwemo ndoa za utotoni mkoani hapa.

Mpango huo umezinduliwa jana Oktoba 13, 2020 katika Kata ya Segese halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na Kamanda wa Polsi wa mkoa huo, ACP Debora Magiligimba, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Shinyanga, likiwamo Shirika la AGAPE, Rafiki SDO, Women Fund Tanzania, Mtandao Jinsia Tanzania (TGNP), UN WOMEN, UNFPA na KOICA.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango makakati huo wa miaka mitano (2020-2025), Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, alisema Serikali ya mkoa huo ni ya kwanza hapa nchini kati ya mikoa 26 kuzindua mpango  mkakati wake wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 

“Mpango huu unaonyesha dira ya mkoa, na kubainisha changamoto zilizopo katika mkoa wetu ambazo zinasababisha matukio haya na kuyafanyia kazi,”alisema Telack. 

Telack alisema kazi ya kuandaa mpango huo imefanywa na viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo mkoani humo, yakiwemo mashirika ya ICS, Women Fund Tanzania (WFT), Rafiki SDO pamoja na AGAPE, ambapo pia wameshiriki kufadhili uzalishaji wa nyaraka za vitabu na uzinduzi wa kitabu hicho cha mpango mkakati. 

"Naiomba sana jamii ya mkoa wa Shinyanga kuachana na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kuacha kuendekeza mila potofu ambazo ni kandamizi zilizopitwa na wakati, badala yake tufanye maendeleo na kukuza uchumi wetu," alisema Telack.


Aidha alisema dhamira ya mkoa huo ni kuona kunakuwepo na usawa wa kijinsia kwenye nyanja zote, zikiwemo shughuli za kiuchumi, pamoja na watoto wa kike kuwa sawa kimasomo na wa kiume, na kuacha tabia ya kuwaozesha ndoa za utotoni na kuzima ndoto zao. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo kutoka Korea Kusini (KOICA), Kyucheol Eo alisema ndoa za mapema na za kulazimishwa zimekuwa tatizo kubwa kwa mabinti, kwani wamekuwa ni wahanga wakubwa kwa kukosa fursa za kielimu na kukosa fedha.

Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sifuni Msangi, aliipongeza Serikali ya mkoa wa Shinyanga kwa kuzindua mpango  mkakati wake wa kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambao ni moja ya utekelezaji wa MTAKUWWA, ambao umelenga ifikapo mwaka 2025 matukio hayo ya ukatili yawe yamepungua ama kuisha kabisa.

Pia Mwakilishi Mkaazi wa UN WOMEN, Juliana Boussard alisema wataendelea kushirikiana ili kufikia lengo la kukomesha vitendo ya ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni.

Hata hivyo tatizo la mimba za utotoni katika mkoa wa Shinyanga lina asilimia 59 na tatizo la ndoa za utotoni asilimia 33.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack (katikati) akizindua rasmi mpango mkakati wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga, zoezi lililofanyika katika Kata ya Segese wilayani Kahama. Kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la KOICA kutoka Korea, Kyucheol EO.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango mkakati wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliofanyika katika kata ya Segese halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga. 
Viongozi mbalimbali na wananchi wa kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga wakimsikiliza mkuu wa mkoa akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango mkakati wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto 
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akizindua rasmi mpango mkakati wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika kata ya Segese wilayani Kahama kulia ni mkurugenzi wa KOICA kutoka Korea Kyucheol EO

Mwakilishi mkaazi wa UN WOMEN Juliana Boussard  akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango mkakati wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliofanyika katika kata ya Segese wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga

Post a Comment

0 Comments