Header Ads Widget

KOCHA KMC AICHIMBA MKWARA YANGA, ATAKA POINTI 3 KESHO KIRUMBA

Wachezaji wa KMC wakijifua kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya Yanga SC utakaopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza

Na Shinyanga Press Club Blog
KUELEKEA mchezo wa kesho (Jumapili) wa raundi ya nane ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Wana Jangwani Yanga SC utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Klabu ya Kinondoni Municipal Council (KMC) FC leo Oktoba 24, 2020 imefanya mazoezi ya mwisho, huku wakitamba kuibuka na ushindi kesho.

Ambapo baada ya mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa KMC FC, Habibu Kondo amesema kuwa kikosi chake kipo tayari kwa mpambano wa kesho dhidi ya Yanga na kwamba anaimani ataibuka na ushindi mnono katika mchezo wa Ligi kuu soka Tanzania Bara.

Habibu amesema kuwa hadi Sasa ameshafanya maandalizi ya kutosha na kwamba hana hofu na mchezo huo kwakuwa anakikosi kipana na kwamba silaha alizonazo zinatosha kuiadhibu Yanga katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Ameongeza kuwa licha ya kwamba kikosi hicho hakikuweza kufanya vizuri katika michezo kadhaa iliyopita lakini tayari ameshazifanyia kazi changamoto zilizopelekea kupoteza kwa michezo hiyo.

"Tumekuja mwanza kutafuta alama tisa katika michezo mitatu tuliyonayo, kesho tunachukua alama tatu kwa Yanga halafu tunaenda kuchukua kwa Gwambia, Biashara na hivyo tukirejea Jijini Dar es Salaam tunarudi kwa kishindo kutokana na ushindi ambao tutakuwa tumeupata" amesema Kocha Habibu.

"KMC FC kesho inacheza mchezo wake wa mzunguko wa nane katika msimu wa Ligi kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Yanga na kwamba kikosi chote kipoimara katika mpambano huo sambamba na wachezaji kuwa na morali nzuri ya mchezo," ameongeza Kocha Habibu.

Wakati huo huo Afisa Habari na Mahusiano wa Timu hiyo ,Christina Mwagala amesema kuwa katika mchezo huo wamejipanga vizuri katika suala zima la uuzwaji wa Tiketi na kwamba hakutakuwa na changamoto zozote katika mchakato huo.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa mpambano huo unakuwa mzuri, uongozi umejipanga na kwamba mageti yote yatakuwa wazi kuanzia saa 1.00 asubuhi na hivyo kila geti litakuwa na wahusika wanaokata Tiketi hizo.
Wachezaji wa KMC wakijifua kwenye uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza 
Mashabiki wakishuhudia mazoezi ya timu ya KMC
Mshambuliaji wa KMC, Hassan Kabunda akikokota mpira wakati wa mazoezi hayo
Mazoezi yakiendelea

Picha na Christina Mwagala



Post a Comment

0 Comments