Header Ads Widget

DADA AMCHOMA MDOGO WAKE AKIMTUHUMU KUTOKA KIMAPENZI NA SHEMEJI AMBAYE NI MWALIMU


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Damian Masyenene – Shinyanga 
VISA vya kushtua na kuvuta hisia za watu vinaendelea kuchukua nafasi na kuripotiwa katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga, ambapo leo Oktoba Mosi, 2020 Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia Meckrida Masesa (25) mkazi wa Chela kwa kosa la kumjeruhi mdogo wake aitwaye Magreth Masesa (15) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Baloha. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema kuwa mtuhumiwa alimjeruhi mdogo wake kwa kumuunguza sehemu za usoni, mashavuni na mapajani kwa kutumia kisu cha moto. 

Kamanda Magiligimba amesema tukio hilo lilitokea Septemba 28, 2020 saa 11 jioni katika kijiji na Kata ya Chela, halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, ambapo Mwanafunzi huyo (Magreth) alijeruhiwa kwa kuunguzwa na kisu cha moto na mtuhumiwa huyo ambaye ni dada yake wakiwa nyumbani kwa mtuhumiwa. 

Ambapo chanzo kilitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi baada ya dada yake huyo kumtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na shemeji yake ambaye ni mume wa mtuhumiwa huyo aitwaye Joseph Masolwa ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Chela. 

“Mtuhumiwa alikiweka kisu hicho kwenye moto kwanza na kisha kuanza kumjerui mhanga. Majeruhi anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Lunguya na hali inaendelea vizuri,” amesema. 

Hivyo, Kamanda Magiligimba ametoa wito wenzi/wanandoa kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wapeleke matatizo/migogoro yao ya ndoa kwenye ofisi za dawati la jinsia na watoto, viongozi wa dini, ofisi za ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao. 

Post a Comment

0 Comments