WANAWAKE wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), 
wameiomba Serikali kuingia katika kupambana na ukatili kwa mwanamke hasa
 rushwa ya ngono mahali pa kazi.
Hayo yalielezwa jana jijini Dodoma na Mwenyekiti wa  Kamati ya ushauri 
wa wanawake Taifa wa chama hicho, Beatrice Njawa, wakati akisoma risala 
katika  mkutano wa siku mbili wa viongozi wanawake wa Talgwu kutoka 
mikoa yote nchini.
Njawa alisema vitendo vya rushwa ya ngono bado vipo katika baadhi ya 
ofisi na imekuwa ni changamoto kwao, hivyo wanaiomba Serikali 
kuliangalia jambo hilo kwa umakini.
“Rushwa ya ngono na mfumo kandamizi bado upo kwenye ofisi zetu, 
kupitia Talgwu tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili licha ya kwamba 
kwa sasa limepungua lakini bado lipo katika baadhi ya sehemu,”alisema.
Alisema changamoto nyingine wanayokutana nayo ni uwakilishi mdogo wa 
wanawake katika ngazi ya maamuzi hivyo aliiomba Serikali kuweka mfumo wa
 pamoja kuhakikisha wanawake wanakuwa wengi katika ngazi za maamuzi.
Mwenyekiti huyo alisema changamoto zingine wanazokabiliana nazo ni 
kusitishwa kwa fao la uzazi, afya na usalama mahali pa kazi huku 
akitolea mfano baadhi ya sehemu vyoo kutokuwa rafiki kwa wanawake.
Alisema changamoto nyingine ni mfumo wa kuchagua wategemezi katika 
Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kutokuwa rafiki kwao kwa kupangiwa watu wa 
kupata huduma hiyo.
Kwa upande wa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Tanzania, 
Pendo Berege alisema changamoto zote wamezipokea na watazifanyia kazi.
Alisema kwamba suala la uwakilishi mdogo kwa wanawake katika ngazi  
za maamuzi  wamelijadili na wamekubaliana kwamba uwakilishi utaongezwa 
na kuonekana.
“Wanawake tunaweza tupeane sapoti kwa sababu kufika  tunapopataka ni 
sehemu moja ila kuwa msemaji wa mambo yetu ni jambo lingine, bado 
tunahitaji kuwa na viongozi wanawake haiwezekani katika vyama vya 
wafanyakazi 34 halafu tuna Katibu mmoja tu mwanamke,”alisema.
Naye, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Nchini (Tucta) ambaye pia ni 
Makamu Mwenyekiti wa Talgwu, Tumaini Nyamhokya, alisema moja ya jambo 
wanalojivunia ni kupambana kuhakikisha darasa la saba wanarudi kazini 
pamoja na punguzo la kodi katika mishahara.
“Tulikaa na Waziri wa Fedha na Mipango vikao kadhaa na baadhi ya mambo yameenda vizuri na yameonekana,”alisema.
Naye, Mwenyekiti wa Talgwu Taifa, Selemani Kikingo, alisema awali 
kulikuwa kunachangamoto ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake lakini kwa 
sasa umepungua kutokana na matatizo hayo  kutatiliwa kuanzia  katika 
ngazi za chini.
                Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
              
 
 
       
 
 
