Header Ads Widget

TAKUKURU NJOMBE YAWAHOJI WAGOMBEA, YAOKOA SH BILIONI 1



Na Amiri Kilagalila,Njombe

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Njombe, imefanikiwa kuwahoji baadhi ya watia nia wa Ubunge wa majimbo, Viti maalum na Udiwani waliokuwa wakiwania nafasi ya kupigiwa kura za maoni katika mchakato uliokamilika hivi karibuni, huku wakihusishwa na vitendo vya rushwa.

Katika taarifa ya kipindi cha mwezi Aprili-Juni, 2020, iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Njombe, Domina Mukama kwa waandishi wa habari, amesema wamefanikiwa kuwafuatilia watia nia wote wakiwa kwenye harakati za kutafuta ridhaa, huku baadhi yao wakihojiwa na kuchukuliwa maelezo yaliyopelekwa katika ngazi nyingine kwa ajili ya maelekezo zaidi.

“Tumeweza kuwafuatilia watia nia wote wa Ubunge wa majimbo,viti maalum na udiwani wakiwa kwenye harakati zao za kutafuta ridhaa kutoka kwa wajumbe watakao wapigia kura, baadhi yao wamehojiwa na hatua stahiki zilichukuliwa dhidi yao,” amesema.

Vile vile amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wameendelea na zoezi la urejeshaji wa fedha zilizokuwa zimefanyiwa ubadhilifu na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika, SACCOS, AMCOS na NJOCOBA.

“Kwa kipindi cha mwezi Aprili –Juni 2020 tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Shs.1,001,060,703.99. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wananchi wote wa mkoa wa Njombe waliojitokeza kulipa madeni na ninaendelea kuwaomba wale wote ambao hawajatimiza kulipa madeni yao waendelee kulipa na kuyamaliza kabisa ili wawe huru.

"Na kwa wale waliotoroka au kukimbia waelewe tu kwamba serikali ina mkono mrefu na tutawakamata popote pale walipo,” amengeza Mukama.