Header Ads Widget

POLISI DODOMA KUDHIBITI UTAPELI KWA WAPAMBE WA WAGOMBEA URAIS VIKAO VYA CCM


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama limejipanga kudhibiti vitendo vya utapeli kwa washiriki uchaguzi kwa kujifanya wapo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (SAC), Gilles Muroto amesema wamejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili mkutano huo ufanyike kwa usalama na amani bila vitendo vya utapeli kutamalaki.

“Jeshi limejipanga kuhakikisha yeyote atakayejaribu kufanya utapeli wa kujifanya yupo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa hawataondoka Dodoma, wajipange kubakia ili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Muroto.

Katika Mkutano Mkuu wa CCM ulioanza leo Julai 7 hadi 12, mwaka huu, utachagua na kupitisha wagombea wa nafasi ya Rais Tanzania Bara na Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

Muroto amesisitiza; “Sitataka kuona vitendo vya utapeli katika mkutano huu unahudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa, viongozi wa Serikali wastaafu, viongozi wa vyama rafiki wa CCM kutoka mataifa mbalimbali duniani na kutoka katika mikoa mbalimbali.”

Muroto amesema mkutano huo unaotarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 3,000 hatapenda kuwaona watu wanaotaka kutenda vitendo vya kitapeli  kwa kujifanya wapo karibu na viongozi.

Amesema uzoefu unaonesha kwamba katika mikutano kama hiyo wamekuwa wakihudhuria watu mbalimbali wakiwemo wapambe wa wagombea, familia za wagombea, wapiga debe, wajasiliamari, lakini pia wanakuwepo watu wabaya ambao wanatumia fursa hiyo kutekeleza azma yao ya kitapeli.

Muroto amesema makundi hayo ambayo yanapanga kufanya vitendo vya kihalifu yasije yakaingia katika mtego ambao hawakutarajia, jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kulinda vitendo hivyo vya kitapeli visitokee.