Mkuu wa Chuo cha VETA mkoani Shinyanga, Abrahamu Mbuguni
Na chibura Makorongo.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Shinyanga, wanaosomea kozi ya udereva wa mabasi na maroli, wameiomba Serikali kupeleka magari hayo chuoni hapo ili kuwapa nafasi zaidi ya mafunzo ya vitendo.
Wanafunzi hao wamesema licha ya Serikali kufanya jitihada kubwa za kutoa fursa kwa vijana, hususan wasichana kujiunga na vyuo vya ufundi, bado kuna changamoto ya ukosefu wa mabasi na maroli ya kufanyia mafunzo ya vitendo.
Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo, mwanafunzi wa kozi hiyo, Mary Jacksoni, alisema kuwa mafunzo wanayopata ni mazuri, lakini ukosefu wa magari makubwa ya mafunzo unawapunguzia uzoefu unaohitajika kazini.
Alisema hivi sasa wasichana wameanza kupata nafasi nyingi za ajira katika sekta ya udereva wa magari makubwa kutokana na kuaminika zaidi na waajiri.
“Tunafikiri kama Serikali itaweka mpango maalum wa kuleta mabasi na maroli, hata kama ni mabovu, mafundi wetu waliopo hapa chuoni wanaweza kuyatengeneza na itakuwa sehemu ya mafunzo ya vitendo,” alisema Mary.
Kwa upande wake, mwanafunzi mwingine Suzana Eliasi alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewaheshimisha wanawake kwa kuwapa nafasi katika fani mbalimbali, ikiwemo udereva wa magari makubwa.
Hata hivyo, alisema changamoto ya ukosefu wa mabasi na maroli chuoni hapo bado ni kubwa, hivyo akaomba magari yaliyoharibika kutoka taasisi za umma kama jeshi na mashirika ya Serikali yakabidhiwe vyuoni kwa ajili ya mafunzo.
“Magari aina ya maroli na mabasi yaliyoharibika yaliyopo jeshini au kwenye mashirika ya umma yanaweza kupelekwa VETA ili wanafunzi wajifunze kwa vitendo. Hii pia itasaidia kupunguza ajali barabarani kwa kuwa madereva watakuwa wamepata mafunzo ya kutosha,” alisema Suzana.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Chuo cha VETA mkoani Shinyanga, Abrahamu Mbuguni, alikiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa magari ya mafunzo, hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotaka kujifunza udereva wa magari makubwa.
Alisema idadi ya wanafunzi, hususan wasichana, imeongezeka hadi wakati mwingine chuo kinashindwa kuwachukua wote.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, hasa wasichana. Wakati mwingine tunapowakataa huonyesha kutoridhika na kudai hii ni fursa iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mbuguni.
Aliongeza kuwa wazo la kupewa maroli na mabasi yaliyoharibika linawezekana, kwani chuo hicho kina uwezo wa kuyakarabati na kuyatumia kwa mafunzo ya vitendo.
“Nilipofika hapa tulikuwa na uhaba wa magari ya mafunzo pamoja na gari la Mkuu wa Chuo, lakini tulianza na magari mabovu tukayakarabati na sasa yanatumika. Hivyo tukipata maroli na mabasi hata yaliyoharibika tunaweza kuyatengeneza na kuyatumia kufundishia,” alieleza.
Aidha, Mbuguni aliwataka wazazi na walezi mkoani Shinyanga kutumia fursa ya uwepo wa chuo hicho kwa kuwapeleka watoto wao kupata mafunzo ya ufundi.
Alisema jambo la kushangaza ni kwamba wanafunzi wengi wanaojiunga na chuo hicho hutoka nje ya mkoa wa Shinyanga, hata kutoka Zanzibar, huku mwitikio wa wakazi wa Shinyanga ukiwa bado mdogo.
“Ni muhimu wazazi na walezi kutumia fursa hii kwa kuwa chuo hiki kinatoa mafunzo yenye tija kwa vijana,” alisema.
