
MATOKEO ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika bandari nchini yameanza kuleta shinikizo chanya la hitaji la miundombinu ya reli, hatua inayotarajiwa kuifungua Tanzania kama kitovu kikuu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hatua hiyo inakuja baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuishauri serikali kuanza uwekezaji wa kuunganisha bandari na reli ili kurahisisha usafirishaji wa shehena zinazoongezeka kwa kasi.
Mjumbe wa kamati hiyo, Profesa Joyce Ndalichako, amebainisha kuwa matokeo ya kufunguka kwa bandari, ikiwemo ile ya Tanga, ni kuongezeka kwa mapato ya serikali, jambo linalotoa msingi wa kujenga Reli ya Kisasa (SGR) kwa ajili ya mizigo.
Profesa Ndalichako alisisitiza kuwa kutumia reli badala ya barabara kutaongeza ufanisi wa kupokea na kusafirisha shehena kutoka bandarini kwenda kwa walaji wa ndani na nje ya nchi.
Uamuzi wa serikali kuanza mpango wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Bandari ya Tanga hadi Musoma unatarajiwa kuleta matokeo yafuatayo ya kiuchumi ikiwamo kupunguza Msongamano.
Kiukweli Bandari ya Tanga sasa inageuka kuwa mkombozi ambapo matokeo ya ujenzi wa reli yatafanya upakuaji na usafirishaji wa shehena kwenda nchi jirani kama DRC, Malawi na Uganda kuwa wa haraka zaidi.
Matokeo ya maboresho ya sasa yamevutia meli nyingi, ambapo kwa sasa meli 14 zinahudumiwa kwa wakati mmoja. Kuwepo kwa reli kutaondoa hitaji la kusubirisha meli (waiting time) na kuifanya bandari hiyo kuwa chaguo namba moja kwa wateja wa kimataifa.
Kutokana na Ongezeko la Uwezo wa Kuhudumia meli Serikali inatarajia matokeo makubwa zaidi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati tatu mpya zenye urefu wa meta 900. Gati hizi zitakuwa na uwezo wa kuhudumia meli nne kubwa kwa wakati mmoja, jambo litakalochagizwa na kasi ya reli ya SGR itakayojengwa.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameeleza kuwa matokeo ya nchi "kufunguka" kiuchumi yanatokana na uwekezaji wa kimkakati ambao unahitaji mfumo wa usafirishaji uliounganishwa (integrated transport system).
Reli ya mizigo itakuwa kiungo muhimu kitakachohakikisha kuwa shehena inayoshushwa bandarini haikai muda mrefu, bali inafika sokoni kwa gharama nafuu na usalama zaidi.
Uchambuzi wa mwelekeo huu unaonyesha kuwa, kuunganishwa kwa Bandari ya Tanga na reli kutaifanya kanda ya kaskazini na ziwa kuwa na mzunguko mkubwa wa kibiashara.
Hii si tu itapunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara, bali itakuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara barani Afrika.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464