.jpg)
Utekelezaji wa Sera ya Afya na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 umepata msukumo mpya kufuatia hatua ya Serikali kuimarisha mashirikiano na sekta binafsi katika kufanikisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.
Katika mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEO Roundtable), Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amebainisha kuwa mkakati huu unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila kukwama kwa gharama kubwa, jambo ambalo ni nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye afya na uzalishaji kuelekea mwaka 2050.
Matokeo ya awali ya sera hii yanaonyesha mafanikio makubwa katika upatikanaji wa huduma, ambapo kwa sasa takribani asilimia 80 hadi 85 ya wananchi wanaweza kufika kituo cha afya ndani ya umbali wa kilomita tano, hali inayopunguza vifo vinavyoweza kuepukika na kuimarisha ustawi wa jamii.
Katika muktadha wa matokeo, Serikali inaendelea kupanua miundombinu ya afya na kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa magonjwa ili kuendana na mahitaji ya kisasa ya kutoa huduma bora. Ushiriki wa sekta binafsi, kama ulivyosisitizwa na viongozi wa CEO Roundtable na Strategis Insurance Group, unaonyesha kuwa afya ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla ni kichocheo cha ufanisi wa taasisi na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Uwekezaji huu unalenga kutengeneza mfumo wa bima ambao hautaishia tu kuwa na kadi mkononi, bali utakaohakikisha upatikanaji wa dawa na huduma stahiki pindi mwananchi anapofika kituoni, ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto za kiutendaji zinazoweza kukwamisha dhamira hiyo njema ya kiserikali.
Mwelekeo wa Dira 2050 unasisitiza kuwa afya bora ni haki ya msingi na nyenzo ya kuleta maendeleo jumuishi, hali inayolazimu kuwepo kwa maboresho endelevu katika huduma za mama na mtoto ambazo zimekuwa kipaumbele cha miaka mingi.
Kwa kuunganisha nguvu kati ya Serikali na wadau wa biashara, mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote unatazamwa kama daraja la kuvuka kutoka kwenye utegemezi wa kulipia huduma kwa fedha taslimu (Out-of-pocket) kwenda kwenye mfumo wa uhakika wa matibabu.
Hii itasaidia kuondoa migongano inayoweza kutokea kutokana na ukosefu wa huduma pindi mwananchi anapokuwa na bima, na badala yake kutengeneza mazingira ambapo kadi ya bima inakuwa na thamani halisi ya matibabu katika ngazi zote za utoaji huduma nchini.