.jpg)
MASHIRIKA ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch (HRW), yamekiri kuwa ripoti zao kuhusu madai ya uvunjifu wa haki za binadamu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025, zilijengeka kwa kiasi kikubwa juu ya taarifa za upande mmoja.
Kukiri huko kumefanyika Machi 12, 2026 mjini Geneva, Uswisi, katika kikao cha pembezoni cha Mkutano wa 61 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Kikao hicho kiliongozwa na Naibu Mkurugenzi wa HRW katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Geneva, Lucy McKernan.
Katika mawasilisho yaliyotolewa na watafiti wa mashirika hayo, ilibainika kuwa taarifa zilizochapishwa kuhusu matukio ya uchaguzi nchini Tanzania zilitokana na mahojiano na nyaraka kutoka kwa vyanzo ambavyo vilitoa maelezo ya upande mmoja, bila kuhusisha kikamilifu maelezo ya Serikali ya Tanzania.
Ilielezwa kuwa, ingawa jitihada za kuwasiliana na serikali zilifanyika kwa njia ya barua, majibu yalichelewa kupatikana, jambo lililosababisha mashirika hayo kutoa ripoti hizo kwa "papara" bila kusubiri ufafanuzi wa upande wa pili.
Hali hiyo ilizua mjadala mzito kutoka kwa wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waliohudhuria kikao hicho. Wawakilishi kutoka nchi za Zimbabwe na Ujerumani walihoji uhalali na weledi wa mashirika hayo kutegemea taarifa ambazo hazikuzingatia uwiano wa pande zote zinazohusika.
“Ni muhimu kusubiri matokeo ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais wa Tanzania ambayo imepewa jukumu la kukusanya ushahidi, maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau wote kabla ya kutoa hitimisho,” walisisitiza baadhi ya washiriki.
Aidha, mjadala huo uliibua hoja ya wajibu wa serikali katika kulinda usalama wa raia na mali zao pale kunapokuwa na viashiria vya hatari au uharibifu. Washiriki walishauri kuwa uwajibikaji unapaswa kugusa pande zote, ikiwemo watu waliotumia lugha za uchochezi ndani na nje ya Tanzania kipindi cha uchaguzi.
Mwakilishi kutoka Ujerumani alitoa onyo kuhusu umuhimu wa kufuatilia kwa karibu mienendo ya uchochezi katika ukanda wa Afrika Mashariki, akitolea mfano mataifa ya Tanzania, Uganda na Kenya, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa mwaka 2027.
Tukio hili linaonekana kuweka doa katika uaminifu wa ripoti za awali za mashirika hayo kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania, huku wadau wa diplomasia wakihimiza matumizi ya vyanzo vya kuaminika na vyenye uwiano katika masuala nyeti ya kitaifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464