` KAMATI YA BUNGE NISHATI NA MADINI YAKOSHWA NA MIRADI YA UMEME SHINYANGA,MEGAWATI 50 ZA UMEME JUA KISHAPU NDANI YA GRIDI YA TAIFA

WANDAMAN HOTEL

KAMATI YA BUNGE NISHATI NA MADINI YAKOSHWA NA MIRADI YA UMEME SHINYANGA,MEGAWATI 50 ZA UMEME JUA KISHAPU NDANI YA GRIDI YA TAIFA


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imeeleza kufurahishwa na kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa jua wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, unaozalisha megawati 50 ambazo tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Subira Mgalu, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.

Amesema hayo leo Machi 13, 2026 wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa umeme wa jua wa Kishapu pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli kilichopo Manispaa ya Shinyanga.
“Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi huu wa umeme wa jua. Tunafarijika kwamba megawati hizi 50 tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa,” amesema Mgalu.

Aidha, ameishauri serikali kuanza mapema utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo itakayozalisha megawati 100 ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini na kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme.
Akizungumza kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, ameipongeza serikali kwa kutumia fedha zake za ndani sh.bilioni 207 kwa ajili ya kupanua kituo hicho.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mradi wa umeme wa Jua wilayani Kishapu, ulianza kutekelezwa mwaka 2023 na awamu ya kwanza umekamilika kwa kuzalisha megawati 50 ambazo tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa.
Amesema, ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo umegharimu Sh. bilioni 118.

“Megawati hizi 50 ni awamu ya kwanza, sasa tunajiandaa kuanza awamu ya pili ambayo itazalisha megawati 100 kwa gharama ya sh. bilioni 216 na tupo katika hatua za kumpata mkandarasi,” amesema Ndejembi.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati, ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika utakaochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi wa umeme wa jua wa Kishapu Emmanuel Anderson, amesema mradi huo una jumla ya paneli za sola 82 na zinatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 25.

TAZAMA PICHA👇👇
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akizungumza.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Nishati na Madini Subira Mgalu akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464