Katika ulimwengu huu, kuna watu wa aina mbili: Wapo wanaotembea kuelekea kule wanakokujua, na wapo wanaotembea kwa sababu tu miguu yao ina nguvu ya kupiga hatua.
Mhandisi Kabenda Balete, mtaalamu wa stadi za maisha na uchumi, amewahi kusema neno moja linalopaswa kuchoma fahamu za kila kijana:"Mafanikio huanza kwa mtu kuwa na maono. Mtu asiyekuwa na maono huwa anaenda popote, na akifika popote anahisi amefanikiwa."
Balete katika mazungumzo yake amehoji vijana akiwataka wajiulize, mara ngapi wameanza siku yao bila ratiba wala lengo, kisha jua linapozama unajisikia umechoka na kuhisi umefanya kazi? Hapo ndipo mtego wa "popote" ulipo. Ukipanda basi lisilo na namba ya kule liendako, dereva akikushusha katikati ya msitu, utasemaje?
Kijana, bila maono, utageuka kuwa msindikizaji wa ndoto za wengine. Utafanya kazi usizozipenda, utaishi maisha usiyoyataka, na mwisho wa siku utajifariji kwa mafanikio madogo yasiyo na tija.
Mhandisi Balete anatukumbusha kuwa kuna tofauti kati ya Kuishi na Kuhakikisha malengo yanatimia. Kuishi ni kitendo cha asili; unakula, unalala, unaamka. Lakini kuishi kwa ajili ya malengo ni nidhamu! Ni kuwa na "Sababu" (Why) ya kwanini unaamka saa kumi na moja alfajiri. Ni kuwa na Sababu ya kwanini unasoma kitabu badala ya kuangalia filamu.
Bila sababu ya msingi, kila kitu unachofanya kitakuwa na nusu ya nguvu zako. Hautakuwa na uchungu na muda wako kwasababu haujui kile unachokitafuta kina thamani gani.
Amsha Kusudi Lako Leo!
Dira ya Taifa 2050 na mapinduzi ya uchumi wa kidijiti tuliyoyazungumzia yanahitaji vijana wenye "Anuani za Makazi ya Ndoto zao." Huwezi kuwa tajiri kama hujui utajiri wako utatokana na nini. Huwezi kuwa mbunifu kama hujui ni tatizo gani unataka kulitatua.
Ni vyema vijana wakaachana na kujijaza ujinga na kujizima data katika mitandao na badala yake wasimame, wachukua karatasi, wandike maono yao na wafafanue sababu ya wewe kuwepo duniani. Ukishakuwa na maono, hata ukikutana na dhoruba, utajua bado hujafika, na utapambana mpaka ufike kileleni.
Ni dhahiri Mhandisi Balete ametoa siri ya wazi. Mafanikio siyo bahati nasibu (lottery); ni matokeo ya mtu aliyekataa kwenda "popote" na akaamua kuelekea "sehemu fulani." Maono ni sumaku—yanavuta rasilimali, watu, na fursa kuelekea kwako.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464