.jpg)
Utekelezaji wa agizo la serikali linalozitaka mamlaka za serikali za mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu umezidi kushika kasi nchini kama sehemu ya mkakati wa kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Katika kutekeleza azma hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph, amevitaka vikundi 24 vilivyopokea mikopo hiyo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kuhakikisha vinatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kukuza biashara na shughuli za ujasiriamali.
Vikundi hivyo vilivyopata mkopo huo wa asilimia 10 vimegawanyika katika makundi ya vijana, wanawake, na watu wenye mahitaji maalum ambapo kwa pamoja vimekabidhiwa jumla ya shilingi milioni 190.
Mkuu wa Wilaya amesisitiza kuwa fedha hizo ni kichecheo kikubwa cha mabadiliko ya kiuchumi kwa makundi hayo ikiwa zitatumika kwa weledi, huku akionya kuwa ni lazima marejesho yafanyike kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine zaidi kunufaika na mfuko huo wa mzunguko.
Mabadiliko haya ya kiuchumi yanayotokana na usimamizi wa asilimia 10 ya pato la halmashauri yanatarajiwa kubadilisha maisha ya vijana na makundi mengine kwa kuwatoa katika utegemezi na kuwafanya kuwa wamiliki wa miradi inayozalisha ajira na kipato.
Kupitia utekelezaji huu wa Mpanda, inadhihirika kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kutumia rasilimali zake za ndani kuhakikisha makundi yote ya kijamii yanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa kupitia ujasiriamali.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464