` KUKABIDHIWA NANAUKA BILIONI 200, KUNAFUNGUA MILANGO YA UWEZESHAJI

KUKABIDHIWA NANAUKA BILIONI 200, KUNAFUNGUA MILANGO YA UWEZESHAJI

Katika kile kinachoonekana kama mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini, Serikali ya Awamu ya Sita imezima rasmi kisingizio cha ukosefu wa mitaji kwa vijana na wanawake baada ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kukabidhi hundi ya shilingi bilioni 200 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka. 

Na hii inafanyika baada ya kipindi kirefu cha kusota na kusubiri kwa hamu fursa za kujikwamua kiuchumi. 

Tukio la kukabidhiwa kwa hundi ya shilingi bilioni 200 jijini Dodoma limekuja kama mkombozi na mwanga wa matumaini kwa maelfu ya wananchi ambao walikuwa wamepoteza mwelekeo kutokana na changamoto za mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara zao. 

Fedha hizi ni sehemu ya ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ikitekelezwa ndani ya siku 100 tu tangu kuingia madarakani , jambo linalodhihirisha kasi ya kipekee ya uongozi wake katika kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma, Dkt. Mwigulu ameweka wazi kuwa utulivu wa nchi ndio msingi mkuu uliowezesha upatikanaji wa mabilioni haya, kwani bila amani hakuna maendeleo wala fursa za kiuchumi zinazoweza kushika kasi. Amewataka vijana kutambua kuwa fursa hii ni tunda la amani iliyopo na hivyo wanapaswa kuithamini kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi.

 Alisisitiza kuwa uwezeshaji huu si zoezi la kawaida la kiofisi bali ni chombo cha mageuzi ambacho kinatakiwa kuwafanya vijana na wanawake kuwa washindani katika soko la ndani na nje ya nchi, huku akionya kuwa serikali haitavumilia yeyote atakayehujumu au kutumia vibaya fedha hizo zilizokusudiwa kuleta tija.

Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa mafanikio ya fedha hizi hayatapimwa kwa idadi ya tarakimu zilizotolewa bali kwa mabadiliko halisi ya maisha ya walengwa, ambapo sasa wizara na taasisi husika zimepewa maelekezo ya kuacha kutoa fedha kama mazoea na badala yake kusimamia matokeo yanayopimika. 

Alieleza kuwa serikali imeweka misingi ya uwazi na uwajibikaji ili kuhakikisha mitaji hiyo inazalisha ajira na biashara endelevu, huku akibainisha kuwa tayari katika kipindi cha muda mfupi kuanzia Novemba 2024, zaidi ya bilioni 66.9 zimekwishatolewa kwa wanufaika elfu 13 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.

Waziri Mkuu,amewataka watendaji na taasisi za fedha zinazoshirikiana na serikali kuondoa mara moja masharti magumu na urasimu usio na tija ambao mara nyingi umekuwa ukiwaogopesha wakopaji wadogo na kuwafanya wakimbilie mifumo isiyo rasmi ya ukopeshaji. Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa ni jambo la kusikitisha kuona benki zikidai dhamana kubwa zisizoendana na kiasi cha mkopo, hatua inayowasukuma watu kwenye mikataba ya kinyonyaji inayojulikana kama "Kausha Damu".

Waziri Mkuu amebainisha kuwa mikopo ya "Kausha Damu" imekuwa ikiwadumaza wananchi kwa riba kubwa zinazowafanya kuwa watumwa wa madeni badala ya kuwaletea maendeleo.

 Agizo hili limetoa mwelekeo mpya kuwa serikali imejipanga kulinda jasho la wananchi wake .

Wakati fedha hizi zikishushwa kwenye wizara husika, amani na utulivu wa nchi vimetajwa kuwa mhimili mkuu uliowezesha mabilioni haya kupatikana na kuanza kugawanywa kwa wananchi. 

 Ni wakati sasa kwa vijana na wanawake kuchangamkia fursa hii adhimu kwa kufika katika taasisi rasmi, kwani kisingizio cha kukosa mtaji kimezikwa rasmi na dhamira ya dhati ya Rais Samia ya kuleta uchumi jumuishi na endelevu kwa kila Mtanzania.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464