` SHINYANGA YAJITOSHELEZA KWA CHAKULA – RC MHITA

SHINYANGA YAJITOSHELEZA KWA CHAKULA – RC MHITA

SHINYANGA YAJITOSHELEZA KWA CHAKULA – RC MHITA

Na Johnson James, SHINYANGA

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuimarisha usalama wa chakula baada ya kuzalisha tani 947,487 za mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, kiasi kinachoufanya mkoa huo kuwa na ziada ya chakula tani 95,003.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, alipokuwa akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, aliyefika mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku moja na kufanya mazungumzo rasmi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mhe. Mhita amesema mahitaji ya chakula kwa Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka ni tani 531,747, hivyo uzalishaji uliopo unauthibitisha mkoa kujitosheleza kikamilifu kwa chakula kwa mujibu wa idadi ya watu kufuatia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hadi sasa.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya kilimo, ambapo pamoja na mazao ya chakula, uzalishaji wa zao la pamba umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka tani 21,599 katika msimu wa 2021/2022 hadi kufikia tani 34,689.22 katika msimu wa 2024/2025.

Kutokana na mafanikio hayo, Mkuu wa Mkoa amemhakikishia Naibu Waziri kuwa mkoa utaendelea kuimarisha matumizi ya maafisa ugani 275 waliopo ili kuhakikisha wakulima wanapatiwa elimu ya kilimo cha kisasa na chenye tija, hatua itakayosaidia kuondokana na kilimo cha mazoea na kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa mapokezi mazuri pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wa mkoa katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Amesema ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga imelenga kukagua bwawa la umwagiliaji la Nyida pamoja na kufanya ukaguzi wa zao la pamba, ili kujionea utekelezaji wa miradi ya kilimo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464