Header Ads Widget

SHIRIKA LA AGAPE LA FUNGUKA MAZITO SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI

Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE John Myola

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKURUGENZI wa Shirika la AGAPE mkoani Shinyanga John Myola, ambao wanatetea haki za watoto, ameizungumzia siku ya mtoto wa kike Duniani, na kueleza changamoto ambazo zinasababisha matukio ya mimba na ndoa za utotoni kuendelea kuwepo mkoani Shinyanga.

Myola akizungumza na Mwandishi wa habari hii, kufuatia leo ni maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani, amesema siku hii ni maalum kwa ajili ya kuikumbusha jamii kumthamini mtoto wa kike na kumpatia haki zake sawa na wakiume.

Alisema wananchi wa mkoa wa Shinyanga ,wanapaswa kumthamini mtoto wa kike, sababu hana tofauti na wakiume, zaidi ya maumbile ya kibailojia, na kuacha kuwabagua kwenye utekelezaji wa mahitaji yao hasa suala la elimu.

"Watoto wakike wana akili sana darasani, mfano watoto ambao ni waathirika wa mimba na ndoa za utotoni tulionao hapa, ambao wanasoma kwa mfumo usiyo Rasmi ufaulu wao ni daraja wa Pili na la tatu, na wengine kwa sasa wapo vyuo vikuu, kidato cha Sita na Tano," alisema Myola.

"Watoto hawa walitaka kuzimwa ndoto zao, lakini sisi Shirika la Agape tukawachukua na kuwaendeleza, na sasa tuna waathirika wa mimba na ndoa za utotoni 63, na wanaendelea na masomo na wako vizuri kitaaluma," aliongeza.

Aidha, alisema wananchi mkoani Shinyanga, wanapaswa kubadilika na kuacha kutomthamini mtoto wa kike, bali wawapeleke shule ili kuja kuwasidia hapo baadae, sababu mtoto wa kike hua hasahau wazazi wake, na siyo kuzima ndoto zao kwa tamaa ya mifugo.

Katika hatua nyingine, alitaja vikwazo ambayo vimekuwa zikisababisha matukio ya mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga kuendelea, ni pamoja na Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, pamoja na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola kuzichukulia kesi za mimba na ndoa za utotoni kama vitega uchumi vyao.

Alifafanua kuwa, Sheria hiyo ya ndoa ya mwaka 1971 ina ruhusu mtoto chini ya umri wa miaka 18, kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au Mahakama, ambapo baadhi ya wanasheria huitumia kuwakinga watuhumiwa ambao ni wateja wao, na kuachiwa huru, jambo ambalo linasababisha matukio hayo kuendelea sababu ya wahusika kutofungwa jela.

Pia, alisema moja ya chombo cha dola (jina limehifadhiwa) baadhi ya watumishi wake siyo waaminifu kabisa, huku akitolea mfano wa kesi moja ya mtuhumiwa kumbaka mtoto, kuwa mmoja wao inasemekana alimwambia mtuhumiwa kuwa atafungwa jela miaka 30, bali atoe Sh.milioni Mbili ili kesi imalizike kimya kimya.

Myola alisema, ili mtoto wa kike apate kulindwa na kupatiwa haki zake za msingi hasa elimu, ni lazima Sheria ya ndoa ifanyie marekebisho ya haraka, kwa kubainisha umri sahihi wa mtu kuolewa miaka 18, ili kutokinzana na Sheria nyingine zinazomlinda mtoto, pamoja na jamii kucha mila na desturi Kandamizi.

Aidha aliiomba Serikali, kuwasaidia msaada wa fedha kupitia mfuko wa benki ya Dunia, wa kusaidia watoto walioathirika na mimba na ndoa za utotoni, ili wapate kuwalipia ada ya shule watoto ambao wanawasomesha, sababu kwa sasa hawapo vizuri kiuchumi, kutokana na kutokuwa na mfadhili, ili watimize ndoto zao.

Nao baadhi ya watoto ambao ni waathirika wa mimba na ndoa za utotoni, walilishukuru Shirika la Agape kwa kutimiza ndoto zao zilitoka kuzimwa kwa kuwapatia elimu tena, huku wakiiomba Serikali kulishika mkono Shirika hilo, ili liendelee kuokoa ndoto za watoto wengi. 
 
Na Marco Maduhu- SHINYANGA

Post a Comment

0 Comments