Na Marco Maduhu, Elizabeth Cosmas, SHINYANGA

Wananchi wa kijiji cha Ikonda na Idodoma wilayani Shinyanga, wamempokea kwa shangwe Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, kutokana na kasi kubwa ya maendeleo ambayo wamewafanyia kwa kipindi kifupi cha ubunge wake.
TAZAMA VIDEO👇👇


Ziara hiyo ya Mbunge Azza katika vijiji hivyo viwili imefanyika leo Septemba 27,2026 kwa nyakati tofauti, kwa kuwashukuru wananchi, pamoja na kusikiliza kero zao na kuzipatia majibu.
Wananchi hao wamesema, kero nyingi ambazo zilikuwa zikiwakabili kwa muda mrefu, baadhi tayari zimeanza kutatuliwa na wamejionea wenyewe, na kumshukuru Mbunge huyo kwa kuendelea kuguswa na maisha ya wananchi na kumuomba aendelee kuwapigania.

Naye Diwani wa Masengwa Nicodemus Simon, amepongeza Mbunge Azza kwa utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi kijiji kwa kijiji, na kwamba katika kijiji cha Ikonda kinakabiliwa na kero mbili kubwa, ambazo ni ubovu wa miundombinu ya barabara, madaraja na maji, na kwamba Mbunge huyo amekuwa msikivu, na kuguswa na matatizo ya wananchi na kuwasemea Bungeni na changamoto zao zimekuwa zikitatuliwa.
“Binafsi na kupongeza Mbunge Azza, kwa kazi nzuri, ndani ya miezi Tisa ya Ubunge wako umeupiga mwingi na maendeleo yanaonekana,” amesema Simon.

Naye Diwani wa Samuye John Ngengeshi, amesema katika Kijiji cha Idodoma walikuwa wamekaa na boma la Zahanati kwa muda mrefu ambalo lilijengwa kwa nguvu za wananchi, lakini ndani ya kipindi kifupi cha Mbunge Azza amepauwa Zahanati hiyo.
“Ndugu sisi Madiwani wa Jimbo la Itwangi tunaraha sana, na wananchi anawawakilisha vizuri na raha mnaziona, miradi ya maendeleo inatekelezea ikiwamo na ujenzi wa miundombinu ya barabara,” amesema Ngengeshi.

Kwa upande wake Mbunge Azza akiwa katika Kijiji cha Ikonda, amesema ndani ya miezi minane ya serikali awamu ya sita katika kijiji cha Ikonda wamepata Kitongoji kimoja cha Kasuguya kwa ajili ya kupatiwa umeme wa REA, lakini hakuna kazi ambayo imefanyika hata kupelekwa nguzo ya umeme, na hivyo kumpigia simu Meneja wa REA Mkoa wa Shinyanga ambaye alitoa majibu kwenye mkutano huo.
Amesema, kwa upande wa kero nyingine ya Maji kwamba hiyo ni ajenda kubwa ya jimbo la Itwangi, na kwamba Jimbo hilo lina vijiji 58, lakini vijiji 34 havina maji kabisa kikiwapo kijiji cha Ikonda, na amekuwa akilisema Bungeni ili wananchi wapate maji.
Amesema, kwa upande wa changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara ikiwamo barabara ya Mwashiku kwenda Igunga ambapo kuna daraja, na suala hilo alilisemea bungeni ili ufanyike utekelezaji kwa kuunganisha daraja hilo upande wa Igunga na Masengwa wilayani Shinyanga.

Ameongeza kwa Barabara ya Isela- Ikonda, kwamba katika Bajeti ya 2026-2027, imeshawekwa kwenye bajeti kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo.

Akizungumzia Zahanati ya Kijiji cha Ikonda kwa upande wa Wodi ya wazazi ,kwamba suala ya ukosefu wa vitanda atakwenda kulisemea ili wapate vitanda.
Akiwa katika Kijiji cha Idodoma Kata ya Samuye, amesema Zahanati ya kijiji hicho kulikuwa na Jengo ambalo halikupauliwa, lakini aliguswa na kuamua kutoa fedha zake mfukoni sh. milioni 10.5 kwa ajili ya kupauliwa, na amefarijika kuona kazi hiyo imefanyika, na sasa atakwenda bungeni kuiomba Serikali ikamilishe Zahanati hiyo na kuanza kutoa huduma.


Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad kesho ataendelea na ziara yake ya kijiji kwa kijiji.

TAZAMA PICHA👇👇

Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wananchi.
Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza na wananchi.

Diwani wa Masengwa Nicodemus Simon akizungumza.
Diwani wa Samuye John Ngengeshi akizungumza.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464