Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza kuwa uamuzi wake wa kufungua soko la dhamana za serikali kwa wawekezaji wote wa kigeni unalenga kupanua wigo wa ushiriki katika masoko ya fedha, kuongeza ushindani, kuvutia mitaji mikubwa kutoka nje na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumzia uamuzi huo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alieleza kuwa hapo awali uwekezaji katika dhamana za serikali ulikuwa umeruhusiwa maalum kwa wawekezaji kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora), lakini kwa sasa benki hiyo imekamilisha mchakato wa kufungua soko hilo kikamilifu kwa wawekezaji wote wasio wakazi duniani kote kupitia marekebisho ya kanuni za usimamizi wa fedha za kigeni.

Gavana Tutuba alifafanua kuwa hatua hiyo inatoa fursa pana za kimataifa za uwekezaji na pia inaruhusu Watanzania wanaotaka kuwekeza nje ya mipaka ya nchi kufanya hivyo kihalali, ambapo mageuzi haya yanakuja ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kimkakati ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuiweka sekta ya fedha katika nafasi nzuri ya kusaidia uchumi.

Kufuatia mabadiliko hayo, BoT ilitangaza rasmi Marekebisho ya Kanuni za Fedha za Kigeni za Mwaka 2026 kupitia Tangazo la Serikali Na. 206 lililochapishwa Julai 17, 2026, ambalo linawaruhusu wawekezaji wote wasio wakazi kushiriki katika dhamana za serikali za muda mfupi na mrefu kwa kuzingatia taratibu na kupitia mawakala wa uwekezaji waliioidhinishwa.

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amewataka wadau wa sekta ya fedha na mawakala wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma na kuwafikia wafanyabiashara wadogo na wakubwa mmoja mmoja ili kuwasaidia kutatua changamoto za kifedha na kuunganishwa na fursa za upatikanaji mitaji, hatua inayotajwa kuwa itasaidia kupunguza gharama za serikali kukopa na kuongeza ushindani kwenye soko la pili la dhamana.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464