TAZAMA VIDEO-KAMPUNI YA MASHATI YATANGAZA NEEMA KWA WAKULIMA WA PAMBA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Kampuni ya ununuzi wa zao la pamba Mashati Oil Investment, imetangaza neema kwa wakulima wa Pamba, kwa kununua pamba yao na kuwalipa pesa papo hapo hakuna mkopo.
TAZAMA VIDEO👇👇
Hayo yamebainishwa leo Julai 2, 2026 mkoani Shinyanga na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Novatus Shirima, ambapo amesisitiza kuwa wamefuata masharti yote ya ununuzi wa zao la pamba, na kwamba mizani zao zimehakikiwa na mamlaka husika.
"Kampuni ya Mashati tuko vizuri na tumejiandaa vyema na soko, tunawakaribisha wakulima wafike kwenye vituo vyetu kuuza pamba, na tunawahakikishia kuwa tunaponunua pamba kwa mkulima, tunampatia pesa yake papo hapo bila kuchelewa," amesema Shirima.
Hatua hiyo ya Mashati Oil Investment inaendana na agizo la Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), ambapo Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi mkoani Shinyanga Renatus Philibert, amezitaka kampuni zote za ununuzi wa Pamba, kuwalipa wakulima fedha zao kwa wakati na kutoingia kwenye madeni.
Pia amezionya Kampuni hizo kutochezea mizani kwa lengo la kumuibia Mkulima na kwamba atakaye kamatwa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kushitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Pamoja na kuwepo kwa soko la uhakika, Bodi ya Pamba imewaonya vikali wakulima kuepuka kuchafua zao hilo wakati wa mavuno ili kutoishusha thamani katika soko la kimataifa.
Aidha, amewataka wakulima, kutovuna pamba ikiwa na vikonyo, kutoweka maji kwenye pamba, kutoipakia pamba kwenye mifuko ya sandarusi.
"Usafi na ubora wa pamba ni msingi muhimu sana wa kuimarisha soko letu kimataifa, tukizingatia kuwa zaidi ya asilimia 70 ya pamba yetu inauzwa nje ya nchi, ambako kuna ushindani mkubwa na nchi zingine," amesema Philibert.
Pia, amewasihi wakulima kutoweka pamba ndani ya nyumba zao kwa matarajio ya kupanda kwa bei, kwani soko la kimataifa halitabiriki na tayari limeanza kushuka.
Kwa upande wao, wakulima mkoani Shinyanga wameonyesha kuridhishwa na msimu huu. Mmoja wa wakulima hao Masanja Dashina, ameishukuru serikali kwa kupanga bei elekezi ya Sh. 1,240 kwa kilo na kusimamia makampuni ili yawalipe kwa wakati.
Dashina ametoa wito kwa wakulima wenzake kuuza pamba yao mapema ili wapate fedha za kujikimu na kununua chakula, huku wakizingatia usafi ili kulinda soko la zao hilo.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Mashati Oil Investiment LTD Novatus Shirima akizungumza.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi mkoani Shinyanga Renatus Philbert akizungumza.
Wakulima wakiuza Pamba yao katika Kampuni ya Mashati Kata ya Mwalukwa wilayani Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
