Header Ads Widget

GULAM AWATAKA BODABODA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI


Diwani wa kata ya Mjini, Gulam Hafidh Mukadam (mwenye shati jekundu) akimjazia mafuta mmoja wa vijana wanaoendesha bodaboda.
 
Na Suleiman Abeid, SHINYANGA

VIJANA wanaojishughulisha na shughuli za usafirishaji abiria kwa kutumia pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda mjini Shinyanga wameshauriwa kuzingatia sheria za barabarani wakati wote ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea na kuwasababishia madhara wateja wao na wao wenyewe.

Ushauri huo umetolewa jana kwa vijana hao na diwani wa kata ya Mjini Shinyanga Gulam Hafidh Mukadam muda mfupi baada ya kumaliza kikao kifupi kilichoandaliwa na uongozi wa Serikali Kata ya Mjini wakishirikiana na Ofisa Polisi katika kata hiyo kuzungumzia umuhimu wa kuzingatia usalama barabarani.

Gulam amesema lengo la mafunzo mafupi ambayo yametolewa kwa vijana hao ni kuwawezesha kuelewa umuhimu wa sheria za usalama barabarani wakati wote pale wanapotekeleza majukumu yao ya usafirishaji abiria kwa kutumia pikipiki zao.

“Mimi nimekuwa na kikao leo hii asubuhi na vijana wetu wajasiriamali wanaofanya shughuli za usafirishaji abiria kwa kutumia pikipiki maarufu (bodaboda) kwa kushirikiana na wenzangu wa Ofisi ya kata ya mjini, polisi kata na mkuu wa usalama barabara wa wilaya ya Shinyanga kwa lengo la kutoa elimu kwao,”

“Elimu hii imelenga zaidi katika kuhakikisha wanapofanya kazi zao wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kujiepusha na ajali zinazoweza kutokea na kusababisha madhara kwao wenyewe ama abiria wanaowasafirisha, elimu hii tunaamini itawawezesha wawe makini wakati wote,” amesema Gulam.

Kwa upande mwingine diwani huyo ametoa lita moja ya mafuta ya petroli kwa kila kijana ambaye ameshiriki katika kikao hicho cha kuwapatia elimu ili yaweze kuwasaidia katika kazi zao na pia kufidia muda wa zaidi ya masaa mawaili ambao wameupoteza kwa ajili ya kuhudhuria kikao.

“Mafuta haya japokuwa ni machache lakini naamini kwa kiasi fulani yatawasaidia, na hii ni kufidia muda ambao wameupoteza kwa ajili ya kushiriki kikao hiki muhimu cha wao kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya sheria za usalama barabarani,” ameongeza Gulam.

Amesema msaada ambao ameutoa ni miongoni mwa sera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuyasaidia makundi maalumu na yeye atahakikisha atakuwa akiyasaidia makundi maalumu kila wakati kama sera ya chama chake inavyoelekeza na anaamini vijana hao watakuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono Serikali iliyoko madarakani.

Kwa upande wake Ofisa mtendaji katika kata ya Mjini, Simon Mashishanga amesema lengo la kuwapatia elimu ya usalama barabara vijana waendesha bodaboda ni kuwawezesha kuzielewa na kuzizingatia sheria hizo wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

“Nitoe wito kwa vijana wetu hawa waendelee kujishughulisha na shughuli hizi katika kuendesha maisha yao, wajiepushe na kushiriki katika matendo yoyote yale ya uvunjifu wa amani, na pia watusaidie kutoa taarifa pindi pale wanapobaini kuwepo viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani wakati wakitekeleza majukumu yao,” anaeleza Mashishanga.

Naye Ofisa Polisi katika Kata ya Mjini, Swalo Mgaya amemshukuru diwani Gulam kwa hatua yake ya kuagiza kufanyika kwa kikao kwa vijana waendesha bodaboda kwa lengo la kuwapatia elimu ya Sheria za usalama barabarani ambayo anaamini itawasaidia kwa kiasi fulani pale wanapofanya kazi yao ya usafirishaji wa abiria.

Baadhi ya vijana ambao wameshiriki kikao hicho wameushukuru uongozi wa Serikali katika kata ya mjini pamoja na diwani Gulam kwa maamuzi waliyoyachukua ya kuwapatia elimu juu ya usalama barabarani ambapo wamesema pamoja na kuzielewa baadhi ya sheria lakini kuna mambo wameongezewa kupitia elimu iliyotolewa.

“Tunashukuru mheshimiwa diwani kwa kutuita sisi wajasiriamali hususani sisi bodaboda katika kata ya mjini, tumepata elimu, elimu hii imekuwa ni chachu kwetu itakayotuwezesha kufanya kazi zetu kwa umakini mkubwa,”
“Lakini hatua budi kumshukuru kwa uamuzi wake wa kutupatia mafuta lita moja kila mmoja, kwa kweli ameonesha jinsi gani anavyotujali sisi vijana wake, tunachoahidi kwao ni kuhakikisha tunazingatia suala zima la usalama barabarani wakati wote tunapotekeleza kazi zetu,” anaeleza Omari Abdalah.
 
 Diwani wa kata ya Mjini, Gulam Hafidh Mukadam (mwenye shati jekundu) akimjazia mafuta mmoja wa vijana wanaoendesha bodaboda mjini Shinyanga.
Diwani wa kata ya Mjini Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafidh Mukadam (mwenye shati jekundu) akizungumza na waendesha bodaboda.
Vijana wanaoendesha bodaboda wakijiandaa kupatiwa mafuta katika moja vituo vya mafuta vilivyopo mjini Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments